Sunday, April 21, 2019

CAG ATEKA MJADALA KWA WIKI MBILI

SHARE
Na MWANDISHI WETU
ZAIDI ya wiki mbili sasa, Mkutano wa 15 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma ukijadili utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 na makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, unaonekana kufunikwa na suala la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mkutano huo ulioanza Aprili 2, 2019, umehusisha uwasilishaji wa makadirio ya bajeti za wizara mbalimbali ikiwamo ile ya Katiba na Sheria ya mwaka 2019/20, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na nyingine.
Hata hivyo, pamoja na wizara mbalimbali kuendelea kuwasilisha makadirio ya bajeti zao, ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita pasipo kuwepo CAG, Prof. Mussa Assad, ndiyo imeonekana kuchukua nafasi katika vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya nchi na hata kujadiliwa kila kona ikihusisha mazungumzo ya watu wa kada tofauti.
Vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi hasa vimeonekana kujikita kuripoti kila kinachoendelea kuhusu sakata hilo hasa ripoti hiyo kuwasilishwa bungeni pasipo uwepo wa Profesa Assad, baada ya Bunge chini ya Spika wake, Job Ndugai, kupitisha azimio la kutofanya naye kazi kwa madai ya kulidharau kwa kuliita dhaifu wakati akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani.
Hadi kufikia jana bado vyombo vya habari vya hapa nchini vilikuwa vikiendelea kuchambua ripoti yake hiyo ya mwaka huu ambayo imeendelea kuibua madudu mengine na ufisadi mkubwa katika fedha za Serikali.
Si vyombo vya habari tu, hata katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwamo Twitter, Instagram, Whatsapp, mjadala wa CAG umeshika kasi kila kukicha kwa watu kuendelea kuujadili hasa msimamo huo wa Bunge.
Baada ya ripoti hiyo kukabidhiwa bungeni, itakumbukwa kuwa Profesa Assad, alizungumza na waandishi wa habari kuhusu yaliyomo kwenye ripoti hiyo na kufafanua neno alilolitumia, ‘dhaifu’ ambalo ndilo kiini cha madai ya Bunge kuwa limedharauliwa kuwa ni la kawaida kwenye fani ya uhasibu.
Baada ya kauli hiyo ya msisitizo kutoka kwa CAG, ilimlazimu Spika Ndugai kuitisha mkutano wa waandishi wa habari kuzungumzia tena suala hilo.
“Tatizo letu ni maneno ambayo Profesa Assad aliyasema kule Marekani na alipowaita waandishi wa habari Dodoma akarudia tena kwamba ataendelea kuyasema maneno hayo. Maneno yale sisi tumeyakataa kuwa si maneno ya kistaarabu hilo ndilo tatizo na si taarifa iliyotolewa,” alisema Ndugai.
Ndugai alimtaka Profesa Assad baada ya msisitizo huo kwenda kujieleza kwa Rais kwani kauli yake inamuweka Rais katika wakati mgumu.
Hata hivyo, kupitia gazeti moja la kila siku lililozungumza na CAG Assad kuhusu ushauri huo wa Spika namna alivyoupokea, Mkaguzi Mkuu huyo alilijibu kwa kifupi kuwa; rejea katiba. 
Wakati hayo yakiendelea pamoja na kulitaja jina la Rais ambaye tayari alikabidhiwa ripoti hiyo na CAG kwa mujibu wa Katiba na kisha kuiwasilisha bungeni kupitia wasaidizi wake, Mkuu huyo wa nchi hajagusia jambo hilo mahali popote na hali ambayo pia imezidi kuibua mjadala.
Rais Magufuli amekuwa akiendelea na ziara zake sehemu mbalimbali nchini na kuzungumza na wananchi kuhusu masuala ya maendeleo huku jambo hilo akilipa kisogo.
MVUTANO HUU ULIANZAJE?
Mgogoro baina ya Profesa Assad na Bunge ulianza baada ya kiongozi huyo kusema kuwa Bunge ni dhaifu kwa kile alichodai kuwa limeshindwa kuisimamia Serikali.
Profesa Assad alitoa kauli hiyo Desemba mwaka jana alipokuwa akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York ambapo alisema Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo Serikali.
Kauli hiyo ilizua mjadala na Januari mwaka huu, Spika Ndugai alilieleza Bunge kuwa Profesa Assad alionesha dharau kubwa dhidi ya mhimili huo na kumtaka aende mbele ya kamati kwa hiari yake, ama apelekwe kwa pingu.
Januari 21, Profesa Assad, alihojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo ilimtia hatiani kwa tuhuma za kudharau chombo hicho.
Aprili 2, Bunge liliazimia kutofanya kazi na CAG huku Aprili 10 ripoti za ukaguzi za 2018/2019 CAG zikiwasilishwa bungeni. SOMA ZAIDI
SHARE

Author: verified_user

0 Comments: