Wednesday, April 24, 2019

Makamba: Zuio mifuko ya plastiki palepale

SHARE
MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa  Rais (Muungano na Mazingira ) January Makamba, amesisitiza kuwa  zuio la mifuko ya plastiki litakuwa la  sheria na hivyo hakutakuwa na msalie mtume.
Hayo aliyasema   Dar es Salaam jana katika mahojiano na redio moja.
Alisema hatua ya kupiga  marufuku  mifuko hiyo lengo  lake ni  kulinda afya za wananchi na mazingira.
“Madhara yanayotokana na  matumizi ya mifuko hiyo ni makubwa   na hivyo siyo rahisi  kwa mtu kuona katika hali ya kawaida.
“Wizara itahakikisaha hatua hiyo inafanikiwa bila vikwazo na   wananchi wataendelea kuelimishwa.
“Katika kukabiliana na zuio hili  changamoto ni nyingi ikiwamo kutokuwa na ufahamu mpana wa wananchi juu ya athari zake, lakini tumejipanga kuhakikisha linafanikiwa na hatua muhimu zaidi ni kutoa elimu kwa wananchi.
“Katazo la kitu kama hiki halikosi vikwazo, kelele na hata vitisho kutoka kwa watumiaji na wazalishaji, hivyo tumejipanga kukabiliana na yote hayo,” alisema Makamba.
Alisema elimu ya kutosha itatolewa kuhusu madhara ya mifuko ya plastiki na njia mbadala zitaanza kutumika wakati wa kipindi cha zuio.
“Tumejipanga kiasi cha kutosha juu ya namna ya kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza na jambo muhimu  ni ushirikiano kwa kuwa mazingira ni suala muhimu kwa kizazi cha leo na kesho;  hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuyalinda,” alisema Makamba.
Baraza laTaifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wiki iliyopita lilieleza kuwa litatekeleza kwa ukamilifu agizo la serikali kwa kutumia sheria.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka,   Sheria ya Mazingira na Kanuni zake vinazuia utengenezaji na matumizi ya kitu chochote kinachoharibu mazingira, ikiwa ni pamoja na mifuko ya plastiki.
“Marufuku hii ina maana kubwa sana katika ustawi wa mazingira ya nchi yetu. Usimamizi wa marufuku hii utaanzia ngazi ya mtaa hadi taifa maana katika ngazi zote hizi tuna ofisi za mazingira.
“Tutatumia sheria kwa nguvu zetu zote, bila ubaguzi.  Tutatumia sheria bila kujali nafasi ya mtu katika jamii, cheo, rangi au mahali anakotoka,” alisema.
Marufuku ya matumizi ya plastiki ilitangazwa bungeni na  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kikao cha Bajeti  kinachoendelea   Dodoma na mwisho wa matumizi wa mifuko hiyo ni Juni 1, mwaka huu.
SHARE

Author: verified_user

0 Comments: