Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile amewataka wanasiasa nchini kuacha kuingilia kazi za Kitaaluma katika sekta ya Afya na kuwaomba wawaache wataalam wafanye kazi zao kwa misingi na miiko ya Kitaaluma inayowaongoza.
Ameyasema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, chini ya Kauli Mbiu “Wakunga Watetezi wa Haki za Wanawake”, ambapo alikuwa akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa hivi karibuni kumekuwa na matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa yanayowakatisha tamaa watumishi wa sekta ya afya na baadhi ya viongozi wameanza kuingilia masuala ya kitaalum, hivyo akawaomba ikiwa viongozi hao watakutana na changamoto za watendaji wa afya waishirikishe wizara ya afya ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa taaluma zao.
“Niwaombe sana viongozi wa Serikali na Viongozi wa vyama, masuala ya kitaaluma yanashughulikiwa kitaaluma kama kuna changamoto na wanataaluma ndiyo maana tuna mabaraza ya taaluma na ndiyo maana sisi wizara tupo mtushirikishe, nimelisema hili kwa sababu nimeona sekta imeanza kuingiliwa,” amesema Dkt. Ndugulile.
Aidha, Dkt. Faustine Ndugulile amewataka wakunga hapa nchini kuendelea kuzingatia miiko na misingi ya taaluma yao katika huduma wanazotoa kwa jamii na kuahidi kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaokiuka misingi hiyo kwa kuwa jamii inahitaji heshimu, utu, upendo na kutiwa moyo
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania, Feddy Mwanga ameiomba Serikali kuongeza idadi ya wakunga ili mkunga aweze kutoa huduma kwa kiwango kinachokubalika Kitaifa na kimataifa huku akisisitiza Serikali kuona haja ya kujenga nyumba za wakunga katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinavyoboreshwa na vinavyojengwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa shilingi bilioni saba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali tatu za Wilaya Bariadi, Busega na Itilima ambazo ujenzi wake unaendelea vizuri.
0 Comments:
Post a Comment