SERIKALI
ya Tanzania inajiandaa kuwasilisha bungeni, muswada wa mabadiliko ya
Sheria ya Takwimu, ili “kujiondoa” kwenye kibano cha kunyimwa fedha za
miradi ya maendeleo na nchi wahisani.” Anaripoti Saed Kubenea … (endelea).
Taarifa kutoka ndani ya serikali na mashirika ya fedha ya kimataifa – Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFM) – zinasema, serikali imelazimika kusalimu amri, kufuatia wafadhili hao, kuzuia mabilioni ya dola za Kimarekani kwa Tanzania.
Benki
ya dunia imetenga takribani dola za Kimarekani 1.7 bilioni (karibu Sh.
4.1 trilioni), kwa ajili ya miradi mbalimbali nchini. Hata hivyo, sehemu
kubwa ya fedha hizo, zimezuiwa kutokana na serikali kupitisha sheria
mpya ya Takwimu.
Benki
ya Dunia na IFM wanasema, sheria hiyo inakiuka haki za binadamu na
kuminya uhuru wa wananchi wa kujieleza na ule wa kutoa maoni.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, serikali imepanga kuwasilisha bungeni
marekebisho ya vifungu kadhaa vinavyolalamikiwa na wahisani na wadau
wengine, “ili kujinusuru na kibano hicho cha kunyimwa fedha.”
Muswaada wa mabadiliko ya sheria hiyo, unatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano huu wa Bunge la Bajeti unaoendelea mjini Dodoma.
Taarifa zinasema, muswada huo, utakuja bungeni kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya kwanza, mwezi Juni mwaka huu.
Bunge
la Jamhuri, lilipitisha mabadiliko ya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2018,
katika mkutano wa Bunge wa Septemba mwaka jana. Mabadiliko hayo
yalikumbwa na upinzani mkali kutoka kwa makundi ya wanaharakati na
wabunge wa upinzani.
Hata
hivyo, muswada huo ulipitishwa kwa mbwembwe bungeni, baada ya serikali
kuamua kutumia wingi na wabunge wa chama tawala – Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Pamoja
na mambo mengine, sheria mpya ya Takwimu inapiga marufuku uchakataji wa
taarifa za tawimu na imeweka marufuku ya kusambaza taarifa zote za
takwimu bila ruhusa ya serikali.
Aidha,
sheria inaelekeza kuwa kila anayetoa taarifa za takwimu kuthibitishwa
na serikali, na kwamba ni kosa la jinai kuchakata na kusambaza taarifa
za takwimu bila ruhusa ya serikali.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka jijini Dar es Salaam na makao makuu ya benki
ya dunia nchini Marekani zinasema, benki imekasirishwa na hatua ya
serikali kupitisha sheria hiyo na imeshinikiza kuondolewa mara moja,
baadhi ya vifungu kandamizi vilivyomo kwenye sheria husika.
Mtoa
taarifa wa MwanaHALISI Online ambaye ni mmoja wa maofisa wa ngazi ya
juu wa IFM amesema, Benki ya Dunia imesisitiza, “haitarejesha hata dola
moja ya fedha zake za maendeleo, kabla ya serikali kurekebisha sheria
hiyo.”
Amesema,
uamuzi wa benki hiyo, umetokana na “kujiridhisha kuwa sheria mpya ya
Takwimu, “inaminya uhuru wa wananchi wa kupata taarifa na kinyume na
Katiba ya Jamhuri na mikataba ya kimataifa.”
Vifungu
ambavyo vipo kwenye Sheria ya Takwimu (2018) na ambavyo serikali
imeahidi wahisani kuvifanyia marekebisho, ni pamoja na kifungu cha 24
(A) (2); 24 (B) (1) pamoja na 24 (B) (2).
Serikali imekubali kukiondoa pia kifungu kinachotoa adhabu kwa watu wanaopatikana na hatia ya kukiuka sheria hiyo.
Mtoa
taarifa huyo anasema, kuwasilishwa kwa mabadiliko ya sheria ya Takwimu
katika mkutano huu wa Bunge la Bajeti, ni sehemu ya makubaliano kati ya
ujumbe wa serikali na maofisa wa ngazi ya juu wa benki ya dunia na IFM.
Mazungumzo kati ya pande hizo mbili, yaliyofanyika wiki mbili zilizopita, jijini Washington DC, nchini Marekani.
Anasema,
katika mkutano huo, taarifa zinasema, ujumbe wa Tanzania uliweza
kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa WB anayeshughulikia masuala ya
Afrika, Hafez Ghanem na Mkurugenzi Mtendaji wa benki anayesimamia nchi
za Afrika, Anne Kabagambe.
Fedha
ambazo zimeondolewa na WB kutokana na kuwapo kwa sheria hiyo, ni pamoja
na dola za Marekani 450 milioni, zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya
kusaidia miradi ya TASAF 111 na dola za Kimarekani 300 milioni,
zilizokuwa zitolewe kwa ajili ya mradi wa maji safi vijijini na maji
taka.
Mamilioni
mengine yaliyozuiwa, ni dola za Marekani 400 milioni, zilizokuwa
zimeombwa kwa ajili ya kuongeza ubora wa elimu ya sekondari.
Anasema,
pamoja na kuwapo kwa sheria ya Takwimu, wahisani wamekasirishwa pia na
hatua ya serikali ya kuweka zuio kwa wasichana waliopata mimba wakiwa
shule za Sekondari kuendelea na mfumo rasmi wa elimu.
“Kule
Marekani wakuwa hawa waliwaambia wazi wazi, maofisa wa Tanzania kuwa
upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo inayo gharamiwa
kwa mikopo nafuu ya Benki ya Dunia, haitatolewa iwapo serikali
haitarekebisha kasoro hizo,” ameeleza afisa huyo wa WB.
Anasema,
“serikali imekubali kufanyia marekebisho kasoro hizo, ikiwa ni pamoja
na kuahidi kuwawezesha wasichana waliopata mimba shule za Sekondari
kuendelea na masomo.”
Tangu
kufanyika kwa mabadiliko kwenye sheria ya takwimu, watu kadhaa,
wakiwamo wabunge na taasisi za kitafiti za ndani, zimeshindwa kuchambua
na kuchapisha taarifa tofauti na zile za serikali hasa katika suala tata
la ukuaji wa uchumi wa taifa.
Wakati
serikali ikidai kuwa uchumi wake umezidi kuimarika, baadhi ya wabunge
hasa wa upinzani, wamekuwa wakiituhumu serikali ya Rais John Pombe
Magufuli, kudanganya kwenye taarifa zake za ukuaji wa uchumi.
Baadhi
ya wakosoaji wa serikali kuhusu taarifa zake za ukuaji wa uchumi (GDP
Growth Rate), wanadai kuwa wameshindwa kutoa taarifa mbadala kwa kuogopa
mkono wa sheria, unaotokana na kuwapo kwa sheria hiyo.
Mpaka
sasa, angalau Zitto Kabwe, mbunge kutoka chama cha ACT- Wazalendo,
kutokea jimbo la Kigoma Mjini, mkoani Kigoma, Magharibi mwa Tanzania,
ndiye anayeonekana kutumia kinga ya Bunge, kukosoa serikali kuhusu
taarifa zake za ukuaji wa uchumi (GDP Growth Rate).
Zitto amekuwa akisema bungeni, kuwa uchumi wa nchi umedorora; kuna tofauti kubwa ya kipato kati ya matajiri na maskini.
0 Comments:
Post a Comment