Mume Na Mke
Kuna
sababu nyingi za kibinafsi, kimaadili, kiuchumi na kijamii zinazoonesha
kuwa wakati mwengine kuoa mke zaidi ya mmoja ni jambo lisilobudi.
Kabla
ya kulieleza jambo hili ni vyema tukaelewa nini maana hasa ya ndoa
(Nikaah) katika Uislam. Ndoa ni mkataba ('Aqd) wa hiari kati ya mume na
mke wa kuishi pamoja kwa wema na upendo kufuatana na masharti na
taratibu zilizowekwa na sheria ya Kiislam.
Kwani
umuhimu wa ndoa kwa mtazamo wa Uislam ni jambo lililokokotezwa sana
kutokana na umuhimu wake katika kujenga na kuendeleza jamii. Kama Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) Alivyosema katika kitabu Chake kitukufu cha
Qur-aan Suratun-Nuur, Aayah ya 32:
((Na
waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi
wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyeezi Mungu Atawatajirisha kwa fadhila Yake.
Na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua)) [An-Nuur: 32]
Tafsiri yake ni kwamba:
Na waozesheni wajane miongoni mwenu (waungwana) na walio wema katika watumwa wema (wanaume) na wajakazi wenu.
Pia vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema katika Suratun-Nisaa, Aayah ya 3:
((… oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. na mkiogopa kuwa hamuwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu)
Tafsiri:
Oeni walio wazuri miongoni mwa wanawake wawili, watatu na wanne, ikiwa munaogopea uadilifu kwa wanawake hao basi oeni mmoja.
Hii
inadhihirisha kuwa tendo la ndoa lina umuhimu mkubwa katika jamii,
ambazo zimetubainishia kuwa ndoa ni ngao ya kujikinga na kitendo kichafu
cha zinaa.
Mwenyezi Mungu Amehalalisha ndoa na kuitilia mkazo kwa wale wenye uwezo kama tunavyojifunza katika Aayah zifuatazo:
“…na mumehalalishiwa (kwa wanawake) mahari ya hawa muyatafute kwa mali zenu, kwa kuwaoa bila ya kufanya zinaa…” (4:24)
Pia katika surah ya (5:5)
((Leo
mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha waliopewa Kitabu ni
halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na pia wanawake wema
miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa walio pewa Kitabu
kabla yenu, mtakapo wapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya
uhasharati wala kuwaweka kinyumba. Na anayekataa kuamini bila shaka
amali yake imepotea, naye katika Akhera atakuwa miongoni mwa wenye
khasara))
Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba:
“Enyi vijana na atakaeweza kati yenu gharama za ndoa (mahari) na aoe”
Pia katika hadithi nyengine amesema:
'Abdullaah
bin Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema “Enyi kongamano la vijana na aoe
yule alie na uwezo miongoni mwenu, hakika kunainamisha macho (na
matamanio) na kuhifadhi tupu (humzuilia mtu na zinaa)na asiyeweza kuoa
na afunge, Hakika funga hukata matamanio (Al-Bukhaary na Muslim).
Pia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Mmoja
wenu atakapomuona mwanamke kisha akamtamani, hana budi kumuendea mkewe
kwani ana kile alichonacho huyo mwanamke aliyemtamani” (At-Tirmidhy)
Ndoa ni Sunnah lakini itakuwa wajibu kwa mwenye kuweza na akawa anayo matamanio na anaogopa kutumbukia katika zinaa.
Katika suala la kuoa mke zaidi ya mmoja ni jambo lisilo budi, kwa kuangalia mifano kadhaa kama vile:
a) Kama mke ni tasa
Mfikirie
mwanamme ambae amehakikisha kuwa mkewe ni tasa na bado ana hamu ya
kupata mtoto atakayekuwa mrithi wake. Katika hali hii mwanamme huyu
atafanya mojawapo katika haya yafuatayo:
i. Atakaa na kusononeka kwa kukosa mtoto katika maisha yake yote au
ii. Atamuacha huyo mwanamke asiyezaa ili aoe mwengine anayezaa au
iii. Atatembea na mwanamke mwengine nje ya ndoa ili ampatie watoto, japo kisheria si watoto wake au
iv. Ataendelea
kukaa na mkewe kwa mapenzi na furaha kisha aoe mke mwengine
atakaemzalia watoto ambao watakuwa wake kisheria.
Utakuta uchaguzi wa kuoa mke wa pili ndio ulio bora kabisa. Wengi katika jamii ya Kiislam wameoa mke wa pili kwa sababu hii.
b) Kama mke ana maradhi ya kudumu
Mfikirie
tena mwanamme ambaye mkewe ana ugonjwa wa kudumu kwa kiasi kwamba hana
uwezo wa kutekeleza majukumu yake kama mke bila ya shaka mwanamme huyu
atafanya mojawapo kati ya yafuatayo:
i. Atajizuia na matamanio yake ya kimwili kwa muda wote wa maisha yake uliobakia au
ii. Anaweza
kumtaliki, mkewe mgonjwa wakati ambapo anahitajia uangalizi, huruma na
mapenzi ya hali ya juu kutoka kwake, ili aoe mke mwengine atakayetosheleza mahitaji yake au
iii. Anaweza kubakia na mkewe mgonjwa na kufanya uzinifu na wanawake wengine nje au
iv. Ataoa mke wa pili atakayemsaidia kumuhudumia mkewe mgonjwa
Hebu tuzijadili hizi hatua tatu (3) kwa mtazamo wa mafundisho ya Uislam
Hatua
ya kwanza: Inakwenda kinyume na umbile la mwanaadamu. Mwenyeezi Mungu
Analifahamu fika umbile la mwanaadamu ya haja yake ya kutosheleza
matamanio ya jimai na Ameweka utaratibu mzuri wa sheria ya ndoa wa
kutosheleza mahitajio haya ya kimaumbile.
Hatua
ya pili: Ni kinyume kabisa na ubinaadamu, kumuacha mke kwa sababu
amekuwa mgonjwa badala ya kumuhudumia kwa upendo na huruma ni kinyume
kabisa na utu. Utaona kuwa hatua ambayo inamuwezesha mume huyu aendelee
kumtunza mkewe kwa huruma na wakati huo huo aweze kutosheleza mahitajio
yake ya kimaumbile kwa utaratibu mzuri wa heshima ni kuoa mke wa pili
c) Wanawake wajane
Wajane
ni wanawake waliofiwa na waume zao, hakuna jamii isiyokuwa na wajane na
idadi yao huongezeka zaidi wakati wa vita ambapo wanaume wengi huuliwa
vitani. Je, wanawake hao warudishwe kwa wazazi au walezi wao au kukaa
hivyo hivyo bila ya kukidhi matashi yao ya kimaumbile mpaka wazeeke, au
waachiwe wawe malaya na kuitokomeza jamii kutokana na matatizo mbali
mbali yanayosababishwa na zinaa? Kwa vyovyote vile, njia pekee ya kuwahifadhi wanawake na watoto wao ni hii ruhusa ya kuoa mke zaidi ya mmoja hadi wanne, kwa kufuata masharti yaliyowekwa.
d) Wanawake wakiwa wengi katika jamii
Inatokezea
katika jamii nyingi wanawake kuwa wengi zaidi kuliko wanaume. Katika
jamii hizi, kama tutaweka sheria ya mume mmoja – mke mmoja kama
wanavyodai watetezi wa usawa wa wanawake. Wanawake watakaokosa wa kuwaoa
watakwenda wapi? Watafanyaje ili kukidhi matashi yao ya kimaumbile?
Je,
kama watazuiliwa mpaka wazeeke huoni hii itawaathiri kimwili, na
kifikra na kuwafanya wasiwe watu wenye manufaa katika jamii? Nani
watakaotoa hifadhi kwa wanawake hawa kiuchumi na kimaadili? Ilivyo
katika maadili ya kibinaadamu, kila mwanamke wa kawaida anahitajia kuwa
na mwanamme anayempenda na kumuhurumia, hivyo wanawake hawa watakapokosa
waume wa ndoa watafanya kila hila za kuwashawishi wanaume kwa kuwawekea
mitego mbali mbali kama vile kujipitisha mbele yao wakiwa wamejipodoa
na kujiremba, kutembea mbele yao uchi, kuzurura kwenye majumba ya sinema
n.k. ambayo itawanasa na kuwatumbukiza katika zinaa.
e) Kuhifadhi jamii na zinaa
Matamanio
ya jamii ni katika maumbile na hayaepukiki katika Uislam. Ndoa ni jambo
lililokokotezwa sana kutokana na umuhimu wake katika kujenga na
kuendeleza jamii. Ndoa kwa mtazamo wa Uislam inatarajiwa:
1. Kuhifadhi jamii na zinaa;
2. Kuendeleza kizazi cha mwanaadamu kwa utaratibu mzuri;
3. Kujenga mapenzi, huruma na ushirikiano katika familia;
4. Kukuza udugu na ushirikiano katika jamii.
Kwa hivyo kuoa mke zaidi ya mmoja ni jambo lisilo budi kwa mwanaadamu kama tulivyoeleza katika mada yetu hii ya ndoa.
Wa Allaahu A'alam
Du’aa Ya Mada Husika
Ee
Mwenyeezi Mungu, hakika mimi nakuomba kheri ya (mke) huyu, na kheri ya
maumbile Uliyomuumba nayo, na najilinda Kwako na shari yake na shari ya
maumbile Uliyomuumba nayo.
0 Comments:
Post a Comment