Monday, May 13, 2019

Nyakati Tatu Muhimu Za Kufanya 'Ibaadah Zisikupite Katika Ramadhwaan

SHARE
Image result for RAMADHAN



Japokuwa nyakati zote za siku katika mwezi wa Ramadhwaan ni tukufu, ila nyakati hizi tatu ni muhimu mno za kutekeleza ‘ibaadah kutokana na fadhila zake adhimu.   Mwenye kupenda kuchuma thawabu nyingi asizikose khaswa katika mwezi huu mtukufu Wa Ramadhwaan ambao ni mwezi wenye malipo maradufu.


1-Wakati wa mwanzo:  Baina ya Alfajiri na jua kuchomoza:

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaamrisha kumsabbih katika wakati huu kama Anavyosema:

وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ﴿٣٩﴾
Na sabbih kwa Himidi za Rabb wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa. [Qaaf: 39]
 وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا ۖ  
Na sabbih kwa Himidi za Rabb wako kabla ya kuchomoza jua, na kabla kukuchwa kwake.    [Twaahaa: 130].

Pia, usimulizi uliothibiti kutoka katika Swahiyh Muslim (564/1) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba walikuwa wakibakia macho wakati huo hadi jua kuchomoza kwani ni wakati mja anapogaiwa rizki yake, na ni wakati wenye kheri nyingi. Pia ni wakati unaosababisha kuwa na siha nzuri ya mwili. Kwa ujumla, ni wakati wenye baraka nyingi za kila aina kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba: 

((اللهم بارك لأمتي في بكورها))  الترمذي ، أحمد ، أبو داود ، ابن ماجه 
((Ee Allaah, wabarikie Ummah wangu nyakati za asubuhi mapema)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah na imethibitishwa kuwa ni Hadiyth Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]

Usimulizi huu umetoka kwa Maswahaba kadhaa ambao wameelezea kwamba: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaka kupeleka kikosi au jeshi aliwapeleka mwanzo wa asubuhi." Vile vile wamesimulia kwamba: "Swakhar alikuwa mtu tajiri ambaye alikuwa akipelekea biashara zake mwanzo wa asubuhi na matokeo yake ilikuwa ni kufuzu katika biashara na kupata faida kubwa sana."

Wamesimulia Salafus-Swaalih kwamba Ibn 'Abbaas naye alimkataza mtu kulala nyakati hizo alipomwambia:
   "قُم، أتنام في الساعة التي تقسَّم فيه الأرزاق؟"
"Inuka! Je, unalala katika saa ambayo rizki inagaiwa?"
 
Ibnul-Qayyim (Rahimahu-Allaah) katika 'Zaad Al-Ma'aad' amesema: "Usingizi wa asubuhi unanyima rizki kwani huo ni wakati ambao Muumba anaombwa rizki na wakati wa kugaiwa rizki. Hivyo usingizi unanyima rizki isipokuwa kwa dharura. Usingizi wakati huo pia ni madhara kwa mwili…"  

Faida nyingine kubwa ya kubakia macho ukimdhukuru Allaah wakati huu


عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال: ((مَنْ صَلَّى الْغَدَاةَ فِي جَمَاعَةٍ ثُمَّ قَعَدَ يَذْكُرُ اللَّهَ حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ ، ثُمَّ صَلَّى رَكْعَتَيْنِ ، كَانَتْ لَهُ كَأَجْرِ حَجَّةٍ ، وَعُمْرَةٍ ، تَامَّةٍ ، تَامَّةٍ ، تَامَّةٍ)) رواه الترمذي (586) أخرج الترمذي  صححه الألباني .
Imetoka kwa Anas kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jamaa'ah kisha akakaa anamdhukuru  Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]
Kwa muda wa saa moja na nusu takriban utakuwa umepata thawabu za Hajj na ‘Umrah zikiwa kamilifu. Pindi ukifanya hivyo kila siku kwa mwezi mzima, utakuwa umechuma thawabu za Hajj na ‘Umrah za mwezi mzima. Hizo ni fadhila za siku za kawaida, seuze ukifanya mwezi mtukufu huu wa Ramadhwaan?

Kwa Rahmah ya Allaah (‘Azza wa Jalla) Amejaalia thawabu hizo ziweze kuchumwa tukiwa majumbani mwetu tena kwa wepesi kabisa. Wanaume inawapasa waswali Msikitini kuzipata thawabu hizo kwa kuwa Hadiyth imetaja atakayeswali jamaa’ah. Ama wanawake, wanazipata fadhila hizo hata wakiswali majumbani mwao kama alivyosema Imaam Ibn Baaz (Rahimahu-Allaah) katika Fatwa yake alipoulizwa kuhusu wanawake kama nao watapata fadhila hizo.

Hata hivyo, juu ya kuweko fadhila kama hiyo, tusisahau kuwa haivunji wala haifuti fardh ya kwenda Hajj kwa mwenye uwezo, asije mtu akadhani kufanya hayo kutakuwa kumetengua wajibu wake wa kuhiji au kufanya ‘Umrah.

Tanbihi: Hadiyth hiyo wamekhitilafiana ‘Ulamaa usahihi wake, kuna waliosema ni dhaifu na wengineo wameipa daraja ya Hasan kama Imaam Al-Albaaniy.

Kuna waliosema kuwa inaingia katika mlango wa kumdhukuru Allaah (‘Azza wa Jalla) kwa wingi kama Alivyoamrisha katika Qur-aan khasa katika wakati huo wa kabla kuchomoza jua  [Fataawa Nuwr ‘Alad-Darb lil-‘Uthaymiyn (2/9)] kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا ﴿٤١﴾
Enyi walioamini!  Mdhukuruni Allaah kwa wingi wa kumdhukuru.

وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا ﴿٤٢﴾
Na Msabbihini asubuhi na jioni‏.[Al-Ahzaab 41-42]

Ama Imaam Bin Baaz (Rahimahu Allaah) aliulizwa kuhusu usahihi wa Hadiyth hii akasema: “Hadiyth hii laa baas, kwani inazingatiwa kuwa ni “Hasan lighayrih” na Swalaah hii inapendekezwa baada ya kuchomoza jua na kupanda kwake yaani takriban baada ya robo saa au thuluthi baada ya kuchomoza kwake jua.” [Fataawaa Shaykh Bin Baaz (25/171).

Na Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) alipoulizwa kuhusu Hadiyth hiyo na fadhila zake kuhusu uhakika wa kuwa atakayetenda atapata thawabu kama za Hajj na ‘Umrah au vipi akajibu: “Kwanza Hadiyth hiyo ina shaka, kwani wengi katika ya ‘Ulamaa wameidhoofisha.  Pili, tukichukuliwa kuwa Hadiyth imethibiti basi thawabu zake hazina kiasi, huenda mtu akatenda ‘amali chache lakini thawabu zake zikawa tele kwa sababu thawabu ni fadhila kutoka kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) Humpa Amtakaye.” [Liqaa Ash-Shahriyy (22/74)]


2- Wakati wa pili: Kabla ya Jua kuzama (Magharibi)

Huu ni wakati ambao bado Muislamu yuko katika Swawm na du'aa yake anayoiomba hairudi:

 قال صلى الله عليه وسلم: ((ثَلاثةٌ لا تُرَدُّ دعوتُهم: الصَّائم حتَّى يُفْطِر، والإمام العادِل، ودعْوة المظْلوم)) وروى الترمذي  بسند حسن
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Watu] watatu du'aa zao hazirudi; mwenye Swawm hadi afuturu. Kiongozi muadilifu na mtu aliyedhulumiwa)) [At-Tirmidhiy kwa isnaad nzuri]

Ni fursa kwa Muislamu atumie wakati huo kuomba du'aa wakati huu hasa kwa vile ni wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Amehimiza Atukuzwe kama Anavyosema:

 وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَارِ﴿٥٥﴾
Na omba maghfirah kwa dhambi zako, na sabbih kwa Himidi za Rabb wako jioni na asubuhi. [Ghaafir: 55]

 وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ﴿٣٩﴾
Na sabbih kwa Himidi za Rabb wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa. [Qaaf: 39]
 وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا ۖ  
Na sabbih kwa Himidi za Rabb wako kabla ya kuchomoza jua, na kabla kukuchwa kwake.    [Twaahaa: 130].



3-Wakati wa tatu: Suhuwr - Kabla ya Alfajiri:

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewaaahidi wenye taqwa wapate kuingia Jannah kwa sababu miongoni mwa sifa zao ni kuomba maghfirah wakati wa suhuwr (kabla ya Alfajiri). Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿١٥﴾
Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu. 

آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِينَ﴿١٦﴾
Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani.

كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ﴿١٧﴾
Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha. 

وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿١٨﴾
Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah. [Adh-Dhaariyaat: 15-18]

Kisha wamesifiwa tena kwa sifa kama hiyo pamoja na nyinginezo:

 الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ﴿١٧﴾
Wenye kusubiri na wasemao kweli, na watiifu, na watoaji mali katika njia ya Allaah na waombao maghfirah kabla ya Alfajiri. [Aal-‘Imraan: 17]

Muislamu asiache wakati huo umpite kwani ni wakati muhimu na wenye fadhila na faida kubwa kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Huteremka katika thuluthi ya mwisho ya usiku kutoka ‘Arshi Yake na kufika mbingu ya kwanza kuwatakabaliwa waja Wake yale wanayomuomba kama ilivyotajwa katika Hadiyth:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba du’aa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

Nani miongoni mwetu asiyemhitaji Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kumtakabalia haja zake au kumuondeshea shida zake? Nani asiyekuwa na madhambi ya kuhitaji kughufuriwa? Hivyo usiache wakati huu ukakupita kamwe kufanya ‘ibaadah, ikiwa ni mwezi wa Ramadhwaan au miezi mingineyo.


Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atujaalie tawfiyq ya kudiriki nyakati hizo tatu na kumudhukuru kwa wingi kwa kusoma Qur-aan, kumsabbih, kumhimidi, kumpwekesha na kumtukuza, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  Na tunamuomba pia Atutakabalie na Atujaalie miongoni mwa watakaoepushwa na moto. Aamiyn 
SHARE

Author: verified_user

0 Comments: