Maswali: Nikaah na Shariyah Zake
SWALI:
Aslam Alyekum
Mie
ni binti wa kiislam ambaye niko masomoni nchini Uingereza na nimepata
mchumba muislam huku UK na anataka kunioa, lakini mtihani tulikuwa nao
ni kwamba mie nasomeshwa na wazazi wangu na kwamba wakijua kwamba
ninamchumba na ninataka kuolewa nae watakataa kunilipa ADA ( School
Fees). (Mchumba wangu hana uwezo wa kunilipia).
Je naomba ushauri kama
inawezekana binti kufunga ndoa kisiri bila wazazi wake kujua (au baba
yake kumuodhesha ikiwa yuko hai?). Kusema ukweli huu ni mtihani mkubwa
kwetu kwani uvumilivu wetu kila siku unapata mitihani na tunataka
kufunga ndoa ili tufanye tendo lile kwa halali lakini kama nilivyosema wazazi wangu wakijua mie shule basi tena na bado nahitaji msaada wao kwa miaka miwili iliyobaki ya course yangu.
Naomba nijibiwe swali langu.
JIBU:
Sifa
zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote,
Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na
watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani
nyingi kwa dada yetu aliyeuliza swali hili nyeti katika Dini na ambalo
vijana wengi wanalipuuzia. Ifahamike kuwa ndoa katika Uislamu ina
masharti yake au nguzo zake ambazo zinaifanya iwe halali na yenye
kukubaliwa kisheria. Kukosekana nguzo mojawapo inaibatilisha ndoa hiyo.
Nazo ni kama zifuatavyo
1. Kuwepo kwa walii ambaye ni baba, ikiwa hayuko au amekufa ndugu wa kiume, na kadhalika;
2. Kwa uchache mashahidi wawili waadilifu;
3. Namna ya kufunga ndoa: Ni Walii kumuozesha binti yake huyo mume na mume mwenyewe kukubali;
4. Kutolewa mahari na mume.
Hakuna
ndoa ya siri katika Uislamu, kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) amehimiza kuwa ndoa itangazwe. Na ikiwa ndoa inayoitwa
ya siri ni ile ambayo kwamba mume anaoa mke wa pili lakini hataki mkewe
wa kwanza ajue hilo, basi itasihi ikiwa imetimiza masharti hayo hapo
juu.
Mara
nyingi huwa tunasema nimekutana na mvulana na namuona ameshika Dini,
lakini mara nyingi huwa hatumjui vilivyo. Kwani utakuwa umekutana naye
katika darasa na kupendana kwa kule kuonana tu mara ya kwanza.
Kuwepo
Walii katika ndoa ni kuhakikisha kuwa maslahi ya binti yametimizwa na
kusiwe na udanganyifu wowote. Hii ni kuwa wasichana wanakuwa madhaifu na
Uislamu unataka kuhakikisha kuwa maslahi yao na haki zao hazidhulumiki.
Katika
kadhiya yako hii ni kuwa masharti ya ndoa hayajakamilika na kukaa
pamoja au kuoana itakuwa mnazini na kupata madhambi. Kisha itakuwa taabu
zaidi kwako lau mzazi atakuja kujua kuwa unakaa na mvulana nawe
umemficha. Hiyo shida ambayo hutaki kuipata ndio itakuwa kubwa zaidi.
Hakika ni kuwa huwezi kuliweka jambo hilo
kuwa siri kwa muda wote wa miaka miwili ambayo upo chuoni. Unaweza
kushika mimba au ikafika habari hiyo nyumbani. Utawajibu nini wazazi
kuhusu hilo?
Nasiha
zetu kwako za dhati ni kuwa mwanzo umfahamu zaidi huyo mume. Je, anazo
sifa ambazo zinatakiwa mume wa Kiislamu awe nazo katika Dini, Ibadah,
Maadili na mengineyo au umempenda kwa sababu ya sura zake na mengineyo.
Miaka miwili si mingi na ikiwa huyo mvulana anakupenda kweli, basi
anaweza kukusubiri mpaka umalize. Katika hali hiyo mnaweza mkawa
mnafunga Swawm ya Sunnah ili kupunguza matamanio. Ni lazima msiwe
mnakutana kama
ilivyoagiza Dini ya Kiislamu ili msije mkafanya dhambi ambapo ndio mara
nyingi hutokea. Ukiona huwezi vumilia basi itabidi uzungumze na mzazi
wako ima mama au baba ambaye unaona anaweza kukuelewa kuhusu jambo hilo. Mara nyingi binti huwa anaweza kuzungumza kwa uwazi zaidi na mama ambaye naye anaweza kumueleza baba kuhusu hilo.
Ikiwa wataelewa na kukufahamu basi itakuwa ni kheri lau wamekataa, basi
jipinde katika masomo na InshaAllah tunamuomba Allah Aliyetukuka
Akupatie lenye kheri nawe hapa duniani na kesho Akhera.
Usifanye haraka.
Na Allah Anajua zaidiUMEZISOMA HIZI?
0 Comments:
Post a Comment