KILIO kimeibuka kwenye familia ya Wakili Maneno Mbunda, Mwanasheria wa Hifadhi ya Wanyama ya Arusha kwa kudaiwa kukamatwa na watu wasiojulikana. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).
Wakili Mbunda alitoewaka siku tano zilizopita baada ya kudaiwa kukamatwa eneo USA River jijini Arusha na watu waliojitambulisha kuwa ni askari ambao hawakuwa na mavazi ya askari wakiwa na gari tatu zisizo na namba za usajili (plat number).
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 3 Mei Mwaka 2019, Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, amesema kuwa mtandao huo umesikitishwa na kitendo cha kutoweka kwa wakili huyo bila kufahamika alipo ilhali kuna vyombo vya usalama nchini.
Amesema kuwa huo ni mfululizo wa kutoweka kwa watu mbalimbali wakimo wanahabari, wanaharakati wa haki za binaadamu na wanasiasa.
Ole Ngurumwa amekumbusha tukio la kutoweka kwa Wakili, Philbert Gwagilo ambaye hajulikani alipo kwa miaka minane sasa, Azory Gwanda Mwandishi wa Habari wa gazeti la Mwananchi aliyepotea kwa mwaka mmoja.
“Tunavisihi vyombo vya usalama hususani jeshi la Polisi mkoani Arusha kufanya uchunguzi wa haraka kwa tukio hilo, pia mwajiri wa Wakili Mbunda achukulie umuhimu suala la ushirikiano kwa familia ya Mbunda na kwa jeshi la Polisi katika kuharakisha uchunguzi,” amesema Ole Ngurumwa.
Pia amesisitiza ombi la kuendelea na uchunguzi wa kutoweka kwa Wakili Gwagilo na Gwanda.
Wakati huo huo, Pendo Mbunda ndugu wa Wakili Mbunda aliyekuwepo kituoni hapo (THRDC) huku akibubujikwa machozi amesema kuwa familia hiyo haina Baba wala Mama na kwamba Mbunda ndiye mlezi wa familia hiyo familia hiyo.
Pendo amesema: “Yeye ndiye aliyekuwa akiilea familia hii, mdogo wetu anakabiliwa na mitihani yake ya kumaliza shule wiki ijayo yeye ndiye msimamizi wa familia hii.”
Taarifa zinasema kuwa Mkuu wa Hifadhi ya Arusha ameiambia Familia hiyo kuwa Mbunda yupo salama.
0 Comments:
Post a Comment