Friday, May 10, 2019

Suarez awachana wachezaji wa Barcelona, Ronaldo de Lima naye asiliba kuhusu Messi

SHARE

Mshambuliaji wa klabu ya Barcelona, Luis Suarez amekosoa kiwango cha uchezaji walichokionesha katika mchezo uliomalizika kwa kipigo cha 4-0 dhidi ya Majogoo wa London, Liverpool, hatua iliyozima safari yao kwenye Ligi ya Mabingwa.
Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Uruguay, amewaambia waandishi wa habari kuwa kocha wa timu hiyo, Ernesto Valverde hapaswi kubebeshwa hata punje ya lawama kwa kipigo hicho bali aliwataka wachezaji kuomba radhi kwa jinsi walivyocheza kama vile sio timu moja.
Alifafanua kuwa kipigo cha goli la nne kilikuwa kibaya zaidi, kwani walicheza kama ‘timu ya vijana’ badala ya kucheza kama timu ya wanaume ya kiwango chao.
“Sisi ndio tunaopaswa kulaumiwa kwa kipigo kile, kocha wetu alitupatia mbinu zote kwenye mchezo wa kwanza. Ni sisi wachezaji, tunapaswa kujielewa sisi ndio tunaocheza,” Suarez aliwaambia waandishi wa habari.

“Tunapaswa kuomba radhi kwa mtazamo wetu, hatukuwa timu. Kwa familia zetu, watoto wetu, mashabiki wetu, tunapaswa kuwaomba radhi, haiwezi kuwa hivyo ndani ya dakika chache tunapata kipigo cha magoli mawili! Kwenye goli la nne tulionekana kama timu ya vijana. Tunatakiwa kuelewa ukosoaji wote ambao unaelekezwa kwetu,” aliongeza.
Mchezaji huyo amewataka wachezaji wenzake kutafakari na kujiongeza kwa ajili ya michezo mingine ya ndani baada ya kuukosa ubingwa wakiishia nusu fainali.
Kauli hiyo ya Suarez inafanana na kauli aliyoitoa hivi karibuni mchezaji wa zamani wa Brazil, Ronaldo de Lima ambaye aliwataka mashabiki kuwa na usawa wanapotoa pongezi na lawama. Alisema kuwa anashangaa pale ambapo timu inafanya vizuri sifa zote zinaenda kwa Lionel Messi lakini inapofanya vibaya lawama zote zinaenda kwa kocha Ernesto Valverde. Hivyo, aliwataka mashabiki kuzipeleka lawama hizo kwa Messi kama wanavyomsifia timu inapofanya vizuri.
SHARE

Author: verified_user

0 Comments: