Tuesday, April 23, 2019

Mufti: Waislamu msiwe sehemu ya mifarakano

SHARE
Bakari Kimwanga-DAR ES SALAAM
SHEIKH Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir, amewataka Waislamu nchini kukataa kuwa sehemu ya mifakano kwa jamii na kuwataka kuwa wamoja ili kuleta maendeleo ya dhati.
Hayo aliyasema juzi usiku alipokuwa akizungumza na Kituo cha Redio Imani.
Alisema ni lazima Waislamu wakatae mambo ambayo yanaweza kuleta mifarakano kwani wao ndio wasimamizi wa amani.
“Msikubali kuleta mambo yanayoweza kuleta mfarakano. Sisi Waislamu ndio tunatakiwa tuwe wasimamizi wa amani. Kwa sababu maana ya salamu tunayosalimiana ni kwamba nakupa amani wewe na mali zako na hali zake.
“Kila mmoja wetu asimamie amani, hatutakiwi kuishi ovyo na wasio Waislamu, tukae nao kwa wema,” alisema Mufti Zubeir.
Akizungumza suala la uanachama wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), alisema kila Muislamu ni mwanachama halali kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Bakwata.
“Mwanachama wa Bakwata ni kila Muislamu wa Tanzania aliyetamka La ilaha illallah Muhammad Rasulullah,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu changamoto inayomnyima usingizi, alisema kuwa ni namna ya kulipanga baraza hilo.
“Changamoto kubwa niionayo ni kulipanga Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania, lingine ni suala la elimu na uchumi kwa Waislamu wote.
“Elimu niisemayo ni elimu ya dini iliyo sahihi na elimu ya mazingira. Tunahimiza Waislamu wasome elimu ya dini na mazingira, tunahitaji madaktari, wachumi na mainjinia,” alisema Mufti Zubeir
Akizungumzia kuhusu suala la uhamasishaji wa elimu ya dini kwa jamii, hasa mijini na vijijini, alisema Idara ya Daawa kwa sasa inazunguka nchi nzima na kutoa elimu ya utambuzi kwa Waislamu.
“Idara yetu ya Daawa inazunguka nchi nzima, Waislamu wote nchi nzima wajitambue, wabadilike, waache ya mazoea. Hii ndiyo kaulimbiu yetu. Na hili ni muhimu kwa viongozi wa Bakwata na Waislamu wote nchini kuacha tabia ya kujiona kama wafalme katika maeneo yao,” alisema.
Akizungumza kuhusu ugaidi, alisema kuwa Uislamu si ugaidi wala haufundishi ugaidi.
“Uislamu sio ugaidi wala haufundishi ugaidi. Ni dini nzuri inatutaka kutomdhuru mtu mwingine. Kama Muislamu mmoja akifanya jambo linaloonekana ni ugaidi ni yeye mwenyewe lakini si Uislamu.
“Tumekuwa tunawaeleza viongozi wa Serikali mtu akifanya ugaidi achukuliwe kama kafanya yeye na si kwa ajili ya Uislamu. Pia tunasema ziondoke fikra potofu, ni kwamba si kila jambo baya lifanywalo limefanywa na Waislamu.
“Moja ya kazi za Bakwata sasa ni kujenga uhusiano mzuri wa Waislamu na Bakwata, ili Waislamu waache fikra potofu kuona Bakwata si chombo chao. Kuna sababu za ndani zilizofanya Waislamu wakawa mbali na Bakwata.
“Kwanza Bakwata haijafanya juhudi kuwaweka karibu Waislamu, lakini sasa tunafanya juhudi kubwa. Tumeunda Kamati ya Muungano na taasisi mbalimbali. Lakini pia kuna watu humu nchini wanaishi kwa kuipinga Bakwata na lazima waishi kwa kufanya hivyo,” alisema Mufti
SHARE

Author: verified_user

0 Comments: