Dar es Salaam. Mahakama Kuu Tanzania
imebatilisha vifungu vya Sheria ya Uchaguzi vinavyowapa mamlaka
wakurugenzi wa halmashauri za majiji, miji, wilaya na manispaa kuwa
wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Mei 10,
2019 na jopo la majaji watatu wa Mahakam a Kuu, ambao waliongozwa na
Jaji Atuganile Ngala. Wengine ni Dk Benhajj Masoud na Firmin Matogolo.
Kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2018,
ilifunguliwa na watetezi na wanaharakati wa haki za binadamu na
demokrasia kwa kushirikiana na vyama vya siasa, vilivyowakiwakilishwa na
mwanachama wa Chadema, Bob Wangwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG).
Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi
hiyo, Wangwe ambaye alikuwa mdai pekee alikuwa anapinga wakurugenzi wa
halmashauri za wilaya, manispaa na au majii kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Pamoja na mambo mengine alikuwa akidai
kuwa wakurugenzi hao ni wateule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa CCM, ambacho pia huwa
kinashiriki katika uchaguzi.
Pia alikuwa anadai kuwa sheria hiyo ni
kinyume cha Ibara ya 74 (14 ) ya Katiba ambayo inapiga marufuku mtu
yeyote anayehusika na uchaguzi kuwa mwanachama wa chama chochote cha
siasa na kwamba ana haki ya kupiga kura tu.
Katika uamuzi wake leo, mahakama hiyo
imekubaliana na hoja za mdai dhidi ya hoja za Serikali iliyokuwa
ikitetea wakurugenzi hao kuendelea kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa madai
kuwa suala hilo haliathiri uchaguzi kwa kuwa uteuzi wao ni kwa mujibu
wa sheria.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Ngala alisema
vifungu 7(1) na 7(3) vya Sheria ya Uchaguzi ni vinakiuka Katiba kwa kuwa
vinakwenda kinyume na matakwa ya kikatiba ya uhuru wa Tume ya Uchaguzi.
Kifungu cha 7(1) ndicho kinachowapa mamlaka wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya NEC.
Hata hivyo, akisoma uamuzi huo Jaji
Ngala amesema vifungu hivyo vinakinzana na Katiba ya Nchi kwa kuwa
wakurugenzi ni wateule wa Rais na hawako chini ya tume na kwamba Katiba
inaelekeza Tume yan Uchaguzi iwe huru.
Jaji Ngwala amesisitiza kuwa sheria hiyo haihakikishi kuwa wakurugenzi hao watakuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema wameridhika na ushahidi
uliotolewa na upande wa mdai kuwa wakurugenzi wengi ni wanachama wa CCM
kwa kuwa kuna wakurugenzi 74 ambao orodha yao imewasilishwa mahakamani
ambao ni wanachama wa chama hicho tawala.
Kifungu 7(3) kinaeleza kwamba NEC inaweza kumteua mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi.
Mahakama hiyo imesema kuwa hata kifungu
hicho hakiweki ulinzi kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa huru na kwamba
lazima kuwe na ulinzi kwa kuhakikisha kuwa anayeteuliwa si mwanachama wa
chama chochote cha siasa.
“Kwa hiyo tunatamka kwamba vifungu hivi
ni kinyume cha Katiba ya nchi inayotaka kuwe na uhuru wa tume katika
utekelezaji wa majukumu yake,” amesema Jaji Ngwala.
Akuzungumza baada ya uamuzi huo, Fatme
Karume, ambaye alikuwa wakili wa Wangwe, amesema kwa uamuzi huo sasa
hakuna wasimamizi wa uchaguzi na kwamba itabidi NEC itumie kifungu cha
7(2) cha sheria hiyo kuteua wasimamizi huru.
Karume ameleezea kufurahishwa na uamuzi
wa mahakama kwa kutotoa amri kwa Serikali ya kufanya marekebisho ya
sheria hiyo wala kuipa muda, akisema kwa uamuzi huo kuanzia sasa kifungu
hivyo ni batili.
Amesema kwamba maana yake imevifuta moja kwa moja badala ya kuipa serika nafasi .
“Kwa hiyo nimefurahi sana, sana kwa
uamuzi huu kwa sababu hatukuwa na tume huru kwa kuwa wale waliokuwa na
jukumu la kuhesabu na kuhakikisha kuwa kura ziko salama hawakuwa huru,”
amesema Wakili Karume.
“Kwa sababu hawako chini ya Tume bali wako chini ya Rais na chama tawala.”
Kwa upande wake, Wangwe amesema
amefurahishwa na ushindi huo na kwamba si wake wala Karume pekee, bali
ni wa watu wote wapenda demokrasia na hata wale wasiopenda harakati
hizo.
“Hili ni fundisho kwamba katika
kupigania utawala bora katika nchi, katika kupigania demokrasia katika
nchi hii, ni suala la kila Mtanzania, kila mtu anangalie wapi kuna
mapungufu, sheria gani ambazo ni mbovu, mahakama hizi ziko kwa ajili
yetu,” amesema Wangwe.
0 Comments:
Post a Comment